Year 2000 World Mission Sunday Message: Swahili
UJUMBE WA PAPA YOHANE PAULO II
JUMAPILI YA MISIONI
OKTOBA 22, 2000
Ndugu zangu wapendwa,
1. Adhimisho la kila Mwaka la Jumapili ya Misioni ambalo litafanyika tarehe 22 Oktoba mwaka huu ni mwito wa utambuzi mpya wa mapana ya umisionari wa Kanisa na changamoto muhimu ya kazi ya kimisionari "kwa mataifa" ambayo "ni kazi ya Wakristo wote, majimbo yote, parokia zote, vyama vyote vya kitume na mashirika yote ya Kanisa" (Utume wa Mkombozi, 2).
Mwaka huu siku hii inapata umuhimu wa pekee zaidi kwa vile inaadhimishwa katika mwanga wa sherehe ya Jubilei Kuu, mwaka wa neema, adhimisho la wokovu ambao Mungu wa huruma na upendo anatoa kwa wanadamu wote. Tunaposherekea miaka 2000 tangu Yesu aza1iwe duniani, tunasherekea pia kuza1iwa umisionari wake. Kristo Yesu ndiye Mmisionari wa kwanza na Mpelekwa Mkuu wa Mungu Baba. Umisionari ulioanza tangu Neno alipotwaa Mwili (Umwilisho wake) unaendelezwa na Kanisa kila wakati kwa njia ya kutangaza Injili na ushuhuda kwa mataifa. Jubilei ni wakati mwafaka wa Kanisa lote, shukrani kwa Roho Mtakatifu, kufanya kazi ya umisionari kwa nguvu na bidii mpya.
Kwa hiyo nawaombeni wabatizwa wote kwa namna ya pekee na kuwasihi kwa moyo mkunjufu, kuwa watangazaji wa Injili, kwa ushujaa na unyenyekevu, kwa kuitikia mwaliko wa Bwana, na kufikiria mahitaji ya watu wa wakati wetu huu waume kwa wake. Nawafikiria maaskofu, mapadre, watawa wa kiume na wa kike nanyi waamini; nawafikiria makatekista na wengine wote mnaofanya kazi za kichungaji katika ngazi mbali mbali, ninyi mnaotekeleza kazi ya umisionari "kwa mataifa" kama wito wenu, mkifanya kazi zenu katika magumu mengi. Kanisa linashukuru kwa majitoleo ya wale wote ambao mara kwa mara "wanapanda kwa machozi" (Zaburi 126,6). Wanapaswa kufahamu kwamba juhudi na mateso yao hayatapotea, kwa kweli watakuwa chachu ambayo itafanywa kumea katika mioyo ya mitume wengine kuamsha tamaa ya kueneza Injili. Kwa niaba ya Kanisa nawashukuru na ninaomba mwendelee kudumu katika moyo huu wa ukarimu: Mungu atawapa tuzo kubwa mara dufu.
2. Nawafikiria pia watu wengine wengi ambao wangeweza kuanza au kuongeza juhudi zao kuitangaza "Injili ya Maisha". Kwa njia mbalimbali wote wanaitwa kuendeleza umisionari wa Yesu katika Kanisa. Huu ni wito mtukufu: kila anayetumwa anaungana kwa namna ya pekee na Yesu mwenyewe, hutenda kazi zile za Yesu, na kama Bwana Yesu asemavyo mwenyewe: "Wanaoniamini watafanya kazi nifanyazo mimi; naam, watafanya hata makuu zaidi" (Yohane 4,12). Kila mmoja ameitwa ashiriki kulingana na hali halisi ya wito wake wa maisha. Katika kipindi hiki, kipindi cha neema na huruma, kwa namna ya pekee ninatambua kwamba nguvu zote za Kanisa zinapaswa kuelekezwa kwa uinjilishaji mpya na kwa umisionari wa mataifa. Hakuna muumini wala vyama vya kitume kuweza kuepuka wajibu huu mkuu wa kumtangaza Kristo kwa watu wote (Utume wa Mkombozi, 3). Hakuna hata mmoja wao anayeweza kujisikia au kujifikiria amesamehewa kutoshiriki umisionari wa Kristo ambao unaendelezwa na Kanisa. Kwa kweli huu ni Wakati mwafaka wa kutekeleza agizo la Yesu "Nenendeni nanyi, mkafanye kazi katika shamba la mizabibu" (Matayo 20,7).
3. Je, kwa jinsi gani tunaweza kushindwa kutaja hapa kwa namna ya pekee, kwa upendo na furaha kuu, kuhusu wamisionari wengi, mashahidi wa imani ambao, kama Kristo, wametoa maisha yao, wakamwaga damu yao? Wamekuwa wengi pia hata katika karne ya 20 ambamo "Kanisa kwa mara nyingine limekuwa Kanisa la wafiadini" (Ujio wa Milenia ya Tatu, 37). Ndiyo, fumbo la Msalaba lipo daima katika maisha ya Wakristo. Niliandika katika Barua yangu ya Kitume kwamba, katika historia ya Ukristo wa nyakati zote wafiadini yaani "Mashahidi wa imani" daima wamekuwa wengi na ni wa lazima kwa utangazaji wa Injili" (Utume wa Mkombozi, 45). Pale ndipo maneno ya Mtume Paulo kwa Wafilipi yanakamilika "Maana ninyi mmepewa fadhili ya kumtumikia Kristo si tu kwa kumwamini bali pia kwa kuteswa kwa ajili yake" (Wafilipi 1,29). Mtume huyu anampa moyo Timotheo, mwanafunzi wake kuteseka pamoja naye kwa ajili ya Injili bila kuona haya, kwa msaada wa nguvu za Mungu (Timotheo 1,8). Utume wote wa Kanisa, na hasa umisionari "kwa mataifa" unahitaji mitume wenye moyo wa kudumu mpaka mwisho, waaminifu kwa utume waliopokea, kwa kufuata njia ile aliyopitia Kristo: "njia ya ufukara, utii, utumishi na kujitoa sadaka, hata kufa (Hati Kwa Mataifa, 5). Tunaomba mashahidi wote wa Imani ambao tumewatangaza, wawe mfano na msaada kwa Wakristo wote ili kazi ya kumtangaza Kristo kwa mataifa yote ionekane kama wajibu maalumu usioepukika wa kila Mkristo.
4. Katika kazi hii Mkristo hayuko peke yake. Ni kweli kabisa kwamba hakuna uwiano kati ya nguvu za kibinadamu na ukuu wa kazi ya umisonari. Uzoefu wa kawaida na wa kweli ni kusikia kutostahili kufanya kazi ya jinsi hii. Lakini ni dhahiri pia kwamba "nguvu zetu za kufanya kazi hii zinatoka kwa Mungu ambaye ametufanya wahudumu wa Agano Jipya (2 Wakorinto 3,5b -6a). Bwana haachi kamwe wale aliowaita kwa utumishi wake. " Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. Nendeni basi, mkawafanye watu wa mataifa yote wawe wanafunzi wangu… Nami nipo pamoja nanyi siku zote, naam, mpaka mwisho wa nyakati (Matayo 28,18 -20). Uwepo wa daima wa Bwana katika Kanisa lake, hasa katika Neno lake na Sakramenti zake ni uthibitisho wa nguvu ya umisionari. Leo utume huu unatekelezwa na waume kwa wake ambao wamepata mwonjo wa wokovu katika udhaifu na mapungufu yao na wanatoa ushuhuda huu kwa ndugu zao, wakifahamu kwamba watu wote wameitwa katika utimilifu wa maisha hayo hayo.
5. Kama mlivyokwisha kusema hapo awali, matazamio ya Jubilei Kuu, ambayo tunaadhimisha, yanatulazimu kujitoa zaidi kwa umisionari wa Mataifa, miaka elfu mbili imemalizika tangu umisionari wa Kristo ulipoanza na bado kuna maeneo makubwa ya dunia, tamaduni, mila na desturi ambapo Kristo na Injili yake haijapenya bado. Ni kwa vipi basi tunaweza kushindwa kusikia mwito unaotoka katika hali hii?
Kwa mtu ambaye ameonja furaha ya kukutana na Kristo hawezi kukaa nayo peke yake, anapaswa kuishirikisha kwa watu wengine. Tunapaswa kuitikia mwito wa kutangaza Injili unaosubiriwa kutoka pande zote za duma, mwito huo huo uliomfikia Paulo Mtume katika safari yake ya pili: "Njoo Makedonia ukatusaidie" (Matendo 16,9). Uinjilishaji ni "msaada" aliopewa mwandamu, tangu Mwana wa Mungu alipojifanya Mtu ili kumwezesha mwanadamu kupata kile ambacho yeye mwenyewe asingeweza kupata: "Urafiki wa Mungu na neema, maisha ya kimungu ndani ya roho ya mwanadamu ambayo peke yake yanakidhi matarajio ya ndani kabisa ya moyo wa binadamu. Kwa kumtangaza Yesu wa Nazareti, Mungu kweli na Mtu kweli, Kanisa linafungulia watu wote nafasi ya kuwa miungu na hivi kuwa binadamu zaidi. Hii ndio njia ya pekee ambayo inaweza kuongoza watu duniani kutambua fahari ya mwito wao na kuukamilisha katika wokovu aliotujalia Mungu" (Fumbo la Umwilisho, 2).
Vile vile tunapaswa kuamini kabisa kwamba, uinjilishaji ni utumishi wenye tumaini kubwa kwa binadamu, vile unawaandaa watu kutekeleza mpango wa Mungu ambaye anataka watu wote, waume kwa wake, waungane naye, ili wawe watu wake, ndugu waliofanywa huru kutoka hali zote za uonevu au ugandamizaji na kujazwa na hisia za umoja na ushirikiano.
6. Sasa napenda kuwakumbuka kwa namna ya pekee watendaji wengi wanaofanya kazi ya umisionari "kwa mataifa:" katika nafasi ya kwanza maaskofu na wasaidizi wao yaani mapadre; mashirika ya kimisionari waume kwa wake; makatekista wa nchi za missioni, ambao bila wao Makanisa yanayositawi wakati huu katika nchi hizi hayangelikuweko. (Barua ya Kitume ya Katekesi, 66).
Hati ya Mtaguzo wa Vatican II kuhusu kazi ya umisionari kwa mataifa yasema: "Vivyo hivyo pongezi zetu za dhati ziwaendee makatekista, waume kwa wake ambao kazi ya kimisionari miongoni mwa mataifa inawategemea sana. Wakijawa na roho wa utume na kwa juhudi kubwa, makatekista wanatoa mchango mkubwa na muhimu kwa uenezaji wa imani na ujenzi wa Kanisa (Hati Kwa Mataifa, 17). Wakifanya kazi kwa juhudi kubwa na kwa moyo, kwa hakika wanatoa msaada muhimu kwa wamisionari katika kazi zao nyingi. Mara nyingi kwa kuzingatia uhaba wa mapadre, makatekista wamekuwa na wajibu mkubwa katika maeneo mengi, wakiongoza jumuiya ndogo ndogo, wakiwa wahamasishaji wa sala, wakiadhimisha liturjia ya Neno la Mungu, wakifafanua mafundisho na kupanga kazi za huduma.
Kwa kutambua umuhimu wa kazi zao, malezi yao ni ya lazima: wapate mafundisho ya kina ya imani na mbinu za ufundishaji kwa uangalifu, malezi endelea ya kiroho na ya utume. (Utume wa Mkombozi, 73). Kazi yao ni ile ambayo daima ni ya lazima. Nimatumaini yangu kuwa wajibu huu katika Kanisa lote utazidi kukua. Elimu na malezi kwa makatekista, kama vile kwa wamisionari wote ni wajibu muhimu wa kichungaji ni kama kusema "kugharamia wahudumu."
7. Kazi ya umisionari ni nyingi na bado imebaki kazi kubwa ya kufanya: kwa hiyo ushirikiano wa kila mmoja ni wa lazima. Kwa kweli hakuna mtu aliye maskini hivyo kwamba hana kitu chochote cha kutoa. Tunashiriki katika kazi ya umisionari kwanza kabisa kwa njia ya sala, katika vyumba vyetu vya siri (Matayo 6,6), wakati wa liturjia, kwa njia ya sadaka na matoleo ya mateso yetu kwa Mungu. Hii ni namna moja ya ushirikiano ambao kila mmoja wetu anaweza kutoa. Ni lazima vilevile kutegemeza umisionari na Makanisa yote kiuchumi. Inaeleweka vizuri gana kwamba fedha zinazokusanywa siku hii, chini ya uongozi wa Shirika la Kipapa la Misioni, ni kwa ajili ya mahitaji ya Makanisa yote. Nachukua nafasi hii, kutoa shukrani zangu za moyoni kwa Shirika hili la Kanisa ambalo kwa miaka 74 limetoa utaratibu kwa siku hii wa kuhamasisha roho ya umisionari kwa watu wote wa Mungu, wote wakishiriki ; yaani, kuanzia watoto hadi watu wazima, kuanzia maaskofu hadi mapadre, kuanzia watawa wake kwa waume hadi walei, wameitwa kuwa wamisionari katika jamii zao; wakijitoa pia kwa mahitaji ya Kanisa nzima. Uhamasishaji na ushirikiano wa kimisionari unaoendelezwa na Mashirika ya Kipapa ya Misioni unawasilisha kazi ya umisionari kwa watu wote wa Mungu kama zawadi: zawadi ya kujitoa binafsi, zawadi ya kujitoa kwa mafaa ya roho na mwili kwa faida ya Kanisa lote (Utume wa Mkombozi, 81 ).
Mwaka huu, kwa namna ya pekee, siku hii itakuwa ni sherehe maalumu Roma pamoja na maadhimisho ya Kongamano la Kimisionari la Dunia ambalo litawaleta pamoja washiriki wote wa Mashirika ya Kipapa ya Misioni kutoka pande zote za dunia, wakiwakilisha Makanisa yote ya kila bara, kama ishara ya umoja wa ujumbe wa Yesu wa wokovu. Mimi mwenyewe Mungu akipenda, nitakuwa na furaha ya kuongoza adhimisho hili maalumu.
8. Wapendwa ndugu zangu, naomba maneno yangu yawe ya kutia moyo kwa wale wote wenye moyo wa kimisionari. Kwa kuadhimisha Jubilei ya Mwaka Mtakatifu 2000, Kanisa lote linajitoa hata zaidi kwa ujio wa umisionari mpya. Tunapaswa kuongeza ari yetu ya utume kuwarithia wengine mwanga na furaha ya imani na kwa mantiki hii watu wote wa Mungu wanapaswa kuelimishwa" (Utume wa Mkombozi, 86). Roho wa Mungu ni nguvu yetu! Roho, ambaye anadhihirisha uwezo wake katika utume wa Yesu, aliyetumwa "kuhubiria maskini habari njema ...na kutangaza mwaka wa neema ya Bwana" (Luka 4,18), ameminwa katika mioyo ya waamini (rej.Warumi 5,5) kutuwezesha kuwa mashahidi wa kazi ya Bwana.
Namwomba Bikira Mtakatifu sana, Mama wa Kristo na Mama wa waamini, Mwanamke msikivu kwa Roho Mtakatifu, atusaidie kurudia wakati wote "ndiyo yake" kwa mipango ya Mungu ya wokovu, katika utume wa uinjilishaji mpya.
Kwa moyo wa furaha na upendo kwenu nyote ambao mnafanya kazi za umisionari "kwa mataifa" kwa juhudi bila ya kujihurumia na kwa jumuiya zenu, ninawapeni baraka zangu za pekee za kitume.
Imetolewa Vatikan, Juni 11, 2000
Sikukuu ya Pentekoste
Papa Yohane Paulo II
Imetafsiriwa na Rev. Alfons Ndekimo
Mkurugenzi wa Kitaifa Mashirika ya Kipapa ya Misioni
P. 0. Box 6672
Moshi, Tanzania